Nani kucheza na nani Ulaya? Droo ya Klabu Bingwa Ulaya 2017-18
Uingereza inawakilishwa na timu sita msimu huu. Chelsea, Tottenham, Manchester City, Liverpool, Manchester United na Celtic.
Timu hizo zitafahamu zitakutana na nani katika droo itakayofanyika Monaco leo saa moja usiku saa za Afrika Mashariki.
Droo itakuwa ya timu 32 na itatoa makundi manane.
Real Madrid walishinda Klabu Bingwa Ulaya mwezi Juni mwaka huu mjini Cardiff, na kuwa timu ya kwanza kushinda kombe hilo – katika enzi za Klabu Bingwa- mara mbili mfululizo.
Kuna ‘vyungu’ vinne vyenye timu nane, huku kila timu moja katika chungu ikiunda kundi lake, ingawa timu kutoka chama kimoja cha soka haziwezi kupangwa katika kundi moja.
Mabingwa wa England, Chelsea watakuwa katika ‘chungu’ namba moja, pamoja na Real Madrid, Bayern Munich, Juventus, Benfica, Shakhtar Denotsk, Monaco na Spartak Moscow.
Chelsea, mabingwa wa Klabu Bingwa Ulaya mwaka 2012, wanarejea katika michuano hii baada ya kukosekana kwa msimu mmoja na wamerejea baada ya kushinda EPL chini ya Antonio Conte.
Manchester United nao wameingia baada ya kushinda Ligi ya Europa, chini ya Jose Mourinho, ambaye alishinda Klabu Bingwa Ulaya na Porto mwaka 2004 na mwaka 2010 akiwa na Inter Milan.
Manchester United walioondolewa kwenye michuano hii katika ngazi ya makundi msimu wa 2015-16, wapo katika ‘chungu’ cha pili, pamoja na Manchester City, Barcelona, Atletico Madrid, Paris Saint –Germain, Borussia Dortmund, Sevilla na FC Porto.
Tottenham na Liverpool watakuwa katika ‘chungu’ namba tatu, pamoja na Napoli, Basel, Olympiakos, Anderlecht, Roma, na Besitkas.
Celtic watakuwa ‘chungu’ namba nne pamoja na CSKA Moscow, Qarabag, Sporting CP, APOEL, Feyenoord, Maribor, na RB Leipzig.
Mechi za makundi zitaanza Septemba 12 na 13.
Fainali ya Klabu Bingwa Ulaya itachezwa kwenye dimba la NSK Olimpiyskyi mjini Kiev, Mei 26, 2018.
Droo ya Ligi ya Europa itafanyika Monaco siku ya Ijumaa.
Everton, wanaocheza usiku huu watakuwa na matumaini ya kuungana na Arsenal, ambao hawachezi Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20.