Latest News

Comments

tanganyika we speak the truth always

Sunday, 30 July 2017

HALI MBAYA YA UPATIKANAJI, USAMBAZAJI NA UGAWAJI WA PEMBEJEO KWA WAKULIMA WA KOROSHO

Leo chama chetu kimetoa 'Taarifa juu ya Hali Mbaya ya Upatikanaji, Usambazaji na Ugawaji wa Pembejeo kwa Wakulima wa Zao la Korosho Nchini'. Hali mbaya ambayo inatishia sekta nzima ya korosho nchini (zao linaloingiza fedha nyingi za kigeni kuliko mazao yote ya bishara nchini).

Ili nchi kama yetu iendelee tunahitaji ukuaji wa kilimo (sekta inayoajiri 65.5% ya watanzania wote) kwa kiwango cha 10% kwa miaka mitatu mfululizo, kisha ukuaji wa 6% kwa miaka mingine 10. Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani ukuaji wa umedumaa zaidi, kwa mwaka jana kilimo kikikua tu kwa 0.6%, lakini uzalishaji wa korosho ulikuwa kwa zaidi ya 70%, wakulima wa korosho, hasa watu wa kusini, mlilifuta machozi taifa, mkituingizia fedha za kigeni zaidi ya Dola milioni 340. Inasikitisha sana kwamba Serikali sasa inataka kuwafukarisha, haithamini mchango wenu huu.

Taarifa tuliyotoa leo inahusisha utafiti uliofanywa na Viongozi wa chama cha ACT Wazalendo wa ngazi ya Majimbo katika mikoa mitano ya Lindi, Mtwara, Pwani, Ruvuma na Tanga kupitia mazungumzo yao na wakulima wa korosho katika mikoa hiyo mitano inayolima korosho zaidi nchini kutafiti hali ya upatikanaji, usambazaji na ugawaji wa pembejeo.

Nafarijika mno kuongoza chama cha namna hii, chama kinachojikita katika kuzungumzia masuala ya watu, chama kinachpinga pale inapostahili kupinga na kinachotoa sera mbadala za namna ya kuendesha masuala mbalimbali ya nchi.

Nakushukuru sana Katibu wa Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi wa ACT Wazalendo kwa kuongoza jopo la Viongozi wa majimbo kufanya majadiliano haya na wananchi, nawashukuru viongozi wote wa majimbo mlioshiriki zoezi hili, mmefanya kazi kubwa sana.

Kwa wakulima wote wa Korosho nchini, mchango wenu ni mkubwa mno kwa Taifa hili, wakati huu ambao Serikali inataka kuharibu maisha yenu, zaidi ya Wakulima 600,000, pamoja na familia zenu, ACT Wazalendo itasimama nanyi, itapaza sauti kusemea matatizo yenu, na itayawakilisha mawazo yenu juu ya namna ya utatuzi wa kadhia yenu, hatutawaangusha kwenye hili.

' Achimbuzanga Aiche' (marafiki zenu wamekuja). Tutakuwa pamoja.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Julai 30, 2017

No comments:

Post a Comment

Recent in Sports

3/MICHEZO/post-grid

Recent Post